Shambulio la Nigeria lauwa watu 16

Polisi wamesema kwenye televisheni nchini Nigeria kwamba watu 16 wameuwawa kwenye miripuko kadha na risasi zilizofyatuliwa katika chuo kikuu kaskazini mwa nchi.

Haki miliki ya picha Reuters

Idara za kutoa huduma za dharura zinasema kulitokea miripuko mitatu iliyofuatiwa na risasi kwenye miongoni mwa vyuo vikuu vya kale kabisa na vyenye hadhi nchini Nigeria..chuo cha Bayero mjini Kano.

Taarifa za awali zinasema wanafunzi kadha wanaoshiriki kwenye ibada ya Jumapili asubuhi katika uwanja wa chuo hicho, ndio pengine waliolengwa.

Ulinzi mkali umewekwa sasa, kikosi cha kutegua mabomu kiko huko, na risasi zimesita.

Hakuna aliyedai kufanya shambulio hilo.

Kikundi cha wapiganaji wa kiislamu, Boko Haram, ambacho kinapigana vita dhidi ya serikali, siku za nyuma kimechoma shule, na kinapinga elimu inayotokana na mataifa ya magharibi.