Sanogo hataki kikosi cha ECOWAS

Kiongozi wa mapinduzi yaliyofanywa mwezi uliopita nchini Mali, Kepteni Amadou Sanogo, amekataa uamuzi wa Jumuia ya Afrika Magharibi, ECOWAS, kutuma wanajeshi nchini humo.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Alisema jeshi - ambalo rasmi limekabidhi madaraka kwa serikali ya mpito - halikushauriwa juu ya uamuzi uliofikiwa na viongozi wa nchi za ECOWAS siku ya Alkhamisi huko Ivory Coast.

Wanajeshi wa Mali walifanya rabsha kwenye mkutano baina ya wapatanishi wa ECOWAS na viongozi wa jeshi mjini Bamako, Mali.

Waliizomea ECOWAS na kuweka bunduki zao tayari.

Viongozi wa jeshi la Mali wamekerwa na mpango wa kutuma kikosi cha wanajeshi 3,000 nchini humo, kulinda kipindi cha mpito cha kurejesha serikali ya kiraia na hatimae kuisaidia serikali kupambana na wapiganaji walioteka eneo la kaskazini.

Baada ya ECOWAS kuiwekea Mali vikwazo vya kiuchumi kufuatia mapinduzi, viongozi wa mapinduzi walikubali kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito inayoongozwa sasa na Dioncounda Traore, aliyekuwa mkuu wa bunge.

Lakini inaelekea viongozi wa jeshi bado wana nguvu, na wanaogopa kikosi cha ECOWAS kitapunguza madaraka yao.