Rais Obama azuru Afghanistan

Rais Obama nchini Afghanistan
Image caption Rais Obama nchini Afghanistan

Akihutubia raia wa Marekani kutoka kambi ya kijeshi nchini Afghanistan, rais wa Marekani Barack Obama ameahidi 'kukamilisha kazi' na kumaliza vita nchini humo.

Akizungumza mwaka mmoja baada ya kuuwawa kwa Osama Bin Laden, ameyapongeza majeshi ya Marekani na kuusifu mpango wa kumaliza mapigano.

Bwana Obama aliwasili nchini Afhganistan katika ziara ya ghafla kutia sahihi makubaliano ya siku za baadaye kati ya Afghanistan na Marekani na rais Hamid Karzai, kabla ya mkutano wa kilele wa muungano wa NATO.

Saa chache baada ya hotuba yake, mlipuko mkubwa uliripotiwa kutokea katika mji mkuu Kabul.

Walioshuhudia wanasema mlipuko huo ulitokea mashariki mwa mji huo, ripoti moja ikielezea kwamba ulitokea kwenye barabara ya Jalalabad, ambako kuna kambi kadhaa za kijeshi zinapatikana.

Ziara ya rais Obama na hotuba hiyo kupitia televisheni inakuja wakati waandishi wanasema raia wa nchi hiyo wameanza kukosa subira katika vita vinavyoendelea nchini Afghanistan.

Bwana Obama na Karzai walitia saini makubaliano ya ushirikiano wa miaka 10. Muungano wa NATO, tayari umejitolea kuwaondoa wanajeshi wake kufikia mwaka 2014.

Takriban wanajeshi elfu 23 miongoni mwa wanajeshi elfu 88 waliokuwa nchini humo wanatarajiwa kuondoka mwishoni mwa mwaka huu, huku wanajeshi wote wa Marekani na NATO wakiondoka kufikia mwaka 2014.