Mwanaharakati Uchina ataka kuondoka

Mwanaharakati wa Uchina Chen Guangcheng Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mwanaharakati wa Uchina Chen Guangcheng

Mwanaharakati wa Uchina Chen Guangcheng amesema kuwa anahofia maisha yake na kwamba anataka kuondoka. Amesema hayo saa chache baada ya kuondoka hifadhi katika ubalozi wa Marekani.

Bw Chen amesema aliondoka kwenye ubalozi huo baada ya maafisa wa Uchina kutishia wanachama wa familia yake.

Lakini Marekani imesema haina habari zozote kuhusu vitisho hivyo na kwamba mwanaharakati huyo hakuomba hifadhi wakati wowote.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, yuko mjini Beijing kwa mazungumzo ya kibiashara na usalama na maafisa wa Uchina.

Awali, Bibi Clinton aliunga mkono Bwana Chen, ambaye amekuwa katika kifungo cha nyumbani kwa takriban miaka miwili.

haki za binadamu

Lakini wakati mazungumzo yalipoanza Bibi Clinton hakumtaja kwa jina.

''Marakeni inaamini kuwa hakuna nchi ina haki ya kumyima mtu haki ambayo ni haki ya kila binadamu- au kuadhibu mtu ambaye anatumia haki hizo. Bibi Clinton alisema.

Hapo Jumatano maafisa wa Uchina walishutumu Marekani kwa kuingilia maswala ya ndani ya nchi yao na kutaka Marekani iombe msamaha kwa kumhifadhi Bwana Chen katika ubalozi wao.

Mkutano unaofanyika Uchina ulitarajiwa kuzungumzia Syria na Korea ya kaskazini lakini imeghubikwa na mzozo wa kidplomasia juu ya Bwana Chen.

Bwana Chen amekuwa katika ubalozi wa Marekani kwa wiki moja baada ya kutoroka kutoka kifungo cha nyumbani katika kijiji chake kilichoko katika mkoa wa Mashariki cha Shandong.