Sudan yakubali kusitisha mapigano

Rais wa Sudan Omar al Bashir Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Sudan Omar al Bashir

Jamhuri ya Sudan imekubaliana na mpango wa Muungano wa Afrika (AU) wa kusitisha uhasama na Sudan Kusini, lakini imesema itajilinda iwapo itashambuliwa.

Jumatano iliyopita, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lilizipa nchi hizo mbili hadi Ijumaa kusitisha mapigano, la sivyo ziwekewe vikwazo.

Lakini kumekuwa na ripoti za kuongezeka kwa mapigano.

Sudan Kusini ilisema siku ya Alhamisi kuwa ndege za kivita za Sudan zilishambulia maeneo ya kijeshi katika jimbo la Unity. Sudan Kusini inasema pia ilishambuliwa ardhini.

Serikali ya Khartoum haijasema lolote kuhusu shutuma hizo.

mpango wa AU

Kulingana na mpango wa amani wa Muungano wa Afrika ambao nchi hizo mbili zimeridhia, Sudan na Sudan Kusini pia zitatarajiwa kurudi katika meza ya mazungumzo, katika siku chache zijazo.

Mzozo wa hivi karibuni ulianza mwezi uliopita wakati Sudan Kusini ilipodhibiti eneo linalozozaniwa lenye utajiri mkubwa wa mafuta la hejlig.

Japo Sudan ndio inayodhibiti eneo hilo kwa sasa, nchi hizo mbili bado zinaonekena kuwa huenda zikarejea vitani.