Sudan yazuia msaada kupita

Msaada wahitajika Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Msaada wahitajika

Mkuu wa kundi la waasi la SPLM-North ameiambia BBC kua Sudan ya kaskazini inazuia misaada isiwafike watu walio katika eneo linalodhibitiwa na waasi na hivyo kuhatarisha maisha ya maelfu.

Zaidi ya watu 200,000 wanakabiliwa na hatari ya kukosa mahitaji kama chakula na maji huku tayari wazee na watoto wameanza kufariki katika Jimbo la Blue Nile, kwa mujibu wa Malik Agar.

Mapatano yalitiwa saini mapema mwaka huu baina ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuia ya Mataifa ya kiarabu kuruhusu chakula kifikishwe katika maeneo yenye mgogoro.

Maelfu ya watu wamepoteza makazi yao kwenye mpaka baina ya Sudan mbili.

Zaidi ya raia 70,000 kutoka Blue Nile wanapewa hifadhi na shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa huko Kusini mwa Sudan iliyopata Uhuru mwaka jana.

Haki miliki ya picha msf
Image caption Uhaba wa maji na chakula

Mvutano baina ya nchi hizi zilizogawika mara mbili, na kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2005, vilizuka tena mwezi uliopita na kutishia kugeuka kua vita kamili.

Bw.Agar ametoa mwito wa msaada wa Kimataifa kwa ajili ya hadi watu 200,000 walio katika Jimbo la Blue Nile, hatua chache kaskazini mwa mpaka na Sudan ya kusini.

Mkuu huyo wa SPLM-North amesema kua "hali ni mbaya mno ambapo watu wazima, wazee, waja wazito na watoto wanafariki kila siku.

Bw.Agar, ni mwenyekiti wa SPLM-North na ametaka suhuhisho la haraka.

Mashirika ya kujitolea likiwemo Samaritan's Purse, yamezuru eneo hilo na linasema kua nyumba zilipigwa kwa mabomu na familia zimeshindwa kuendelea na kilimo kutokana na mapigano hivi sasa wamelazimika kutafuta matawi na mizizi ya miti pori kujaribu kunusuru maisha.

Watu wengi wanaishi katika mapango kwenye milima kuepuka mashambulizi kutoka angani, yanayofanyika kila usiku na mchana.

Mapatano ya kuwasilisha msaada wa chakula yalifikiwa miezi mitatu iliyopita, lakini hadi sasa hakuna msaada uliofika kwa sababu Sudan ya kaskazini imefunga njia, amesema Bw.Agar.

Kundi la waasi la SPLM-North linasema linapigana vita katika majimbo ya Kordofan ya kusini na Blue Nile siyo kudai Taifa bali kuipindua serikali mjini Khartoum.

Kundi hili linajiona kama linaloendeleza mwamko wa SPLM la marehemu John Garang linalotawala huko Sudan ya kusini.

Wakati huo huo, Kamishna wa tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na haki za binadamu, Navi Pillay, alitazamiwa kuanza mazungumzo na Rais wa Sudan ya kusini Salva Kiir siku ya jumatano juu ya hali nchini mwake.

Umoja wa Mataifa umeonyesha wasiwasi juu ya ukiukaji wa haki za binadamu wakati mvutano ukiongezeka baina ya Sudan ya kusini na kaskazini.