Sudan yazuia msaada kwa raia wa S.Kusini

Haki miliki ya picha NA
Image caption Watoto wanaotoroka vita nchini Sudan

Madai yamejitokeza kuwa serikali ya Khartoum inazuia msaada kuingizwa katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi ya waasi wa kundi la SPLM_Kaskazini na hivyo kuhatarisha maisha ya raia walio katika eneo hilo.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kiongozi wa waasi wa SPLM-kaskazini kwa BBC .

Zaidi ya watu 200,000 wakiwemo watoto na wazee wako katika hali mbaya na wanahitaji msaada wa dharura katika jimbo la Blue Nile. Kulingana na kiongozi huyo Malik Agar.

Mwafaka uliafikiwa mapema mwaka huu kati ya nchi hizo mbili kwa usaidizi wa Umoja wa mataifa, Muungano wa Afrika na jumuiya ya nchi za kiarabu kukubalia chakula kuingizwa katika maeneo ya mzozo.

Maelfu ya watu wametoroka makwao katika eneo la mpakani kati ya Sudan na Sudan Kusini.

Zaidi ya watu 70,000 kutoka jimbo la Blue Nile wanahudumiwa na shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi nchini Sudan Kusini.

Hali ya taharuki imeghubika nchi hizo mbili zilizopigana vita vya muda mrefu ambavyo viliisha mwaka 2005, na kusababisha hofu ya kuzuka upya mapigano.

Hii leo ndio itakuwa mwisho wa makataa iliyotolewa na baraza la usalama la umoja wa Mataifa kwa nchi hizo mbili kuondoa wanajeshi wao mpakani na kuunda kamati ya wajumbe kutoka pande hizo mbili kuchunguza mpaka huo.

Bwana Agar ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kutoa msaada wa dharura kusaidia takriban watu 200,000 eneo la Blue Nile kaskazini mwa mpaka na Sudan Kusini.

Ameonya kuwa msimu unaokuja wa mvua huenda ukafanya hali kuwa mbali zaidi.