ECOWAS yatishia kurejesha vikwazo Mali

Haki miliki ya picha
Image caption Kapteini Sanogo na Spika wa bunge

Muungano wa kanda ya Afrika Magharibi ECOWAS umetishia kuwawekea vikwazo upya wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Mali kwa kuyumbisha mchakato wa kurejesha utawala wa kikatiba.

ECOWAS iliondoa vikwazo mwezi Aprili pale wanajeshi hao waliporidhia kurejesha utawala wa kiraia.Kanda ya Afrika Magharibi imepinga jaribio la kumuondoa Rais wa mpito nchini Mali Djouncounda Traore.

Bw.Traore, ambaye ni spika wa bunge aliapishwa kama Rais chini ya mpango ambapo jeshi ilikubali kurejesha utawala wa kiraia. Kiongozi wa mapinduzi Kapteini Amadou Sanogo ameitisha kongamano la kitaifa linalojumuisha mashirika ya kiraia ili kuchagua utawala wa mpito baada ya muda wa Bw Traore kumalizika hapo Mei 22.

Utawala huu utasaidia kuandaa uchaguzi wa kidemokrasia. ECOWAS inamtaka Bw.Traore kuendelea kuongoza kipindi cha mpito kwa mwaka mmoja.

Mnamo mwezi Machi, wanajeshi wa nyathifa ya kati wakiongozwa na Kapteini Sanogo walipindua utawala wa Rais Amadou Amani Toure, wakimlalamikia kushindwa kushughulikia uasi kaskazini mwa nchi ambao unaongozwa na Wa-Tuareg.

Baada ya muungano wa ECOWAS kuweka vikwazo, wanajeshi waliopindua serikali walikubali kurejesha utawala wa kiraia ambapo Spika wa bunge Djouncounda Traore alichaguliwa kama Rais wa mpito.

Licha ya kurejesha utawala wa kiraia, wanajeshi hao wameendelea kuingilia siasa na uwongozi wa nchi.