Matatizo yataizonga Afghanistan

Rais Barack Obama ameonya kuwa Afghanistan itakabiliwa na kipindi kigumu katika siku zijazo wanajeshi wa Nato wakiwa wanajiandaa kuondoka nchini humo mwaka wa 2014.

Image caption Obama anasema jeshi la Nato litatoka 2014

Rais Obama amesema hayo kwenye mkutano wa shirika la kujihami la Nato unaoendelea mjini Chicago, nchini Marekani.

Wakati nchi wanachama wa Nato wakijiandaa kuondoa majeshi yao nchini humo mwaka wa 2014, Rais mpya wa Ufaransa Francois Hollande ametangaza kuwa ataondoa majeshi ya nchi yake ifikiapo mwaka wa 2012.

Mwandishi wa masuala ya usalama wa BBC Caroline Wyatt anasema mkutano huo una malengo mawili.

Mwanzo ni kuwaelezea raia wa nchi zao kuwa vita Nchini Afghanistan vinakaribia kuisha na kuwa wanajeshi wao wanarudi nyumbani, na pili kuwapa moyo raia wa Afghanistan kuwa hawata watelekeza baada ya kuondoka.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai ameambia mkutano huo kuwa serikali yake inaelewa majukumu yake.

Mkutano huo unaingia siku ya pili leo ambapo mjadala mkubwa utakuwa kuhusu kiasi cha pesa kinachohitajika kusaidia serikali ya Afghanistan na ni nani atakaye changia fedha hizo.

Zaidi ya viongozi 50 wanahudhuria mkutano huo akiwemo Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari.

Rais Zardari amepangiwa kufanya mkutano na viongozi hao baadae leo kuhusu utaratibu wa Pakistan kufungua njia zitakazo tumiwa na wanajeshi wa Nato nchini Afghanistan kusafirisha bidhaa zao.

Katibu Mkuu wa Nato Anders Fogh Rasmussen amesisitiza kuwa shirika hilo litafuata utaratibu iliowekwa awali wa kuondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan na wala hautaharakishwa.