Uchaguzi unaingia siku ya pili Misri

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mpiga kura Misri

Vituo vya kupiga kura vitafunguliwa tena kwa siku ya pili leo nchini Misri katika uchaguzi wa kwanza huru tangu mapinduzi ya kiraia yaliomuondoa Rais Hosni Mubarak mamlakani miezi 15 iliopita.

Jumla ya wagombea 12 wanawania urais wa nchi hiyo.

Kiasi kikubwa cha wapiga kura milioni 50 waliosajiliwa walijotokeza vituoni hapo jana wakiwa watulivu na wenye furaha.

Baraza kuu la jeshi nchini humo ambalo lilichukuwa utawala baada ya mapinduzi ya kiraia mwezi wa Februari mwaka jana, limeahidi kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki.

Uchaguzi huo umeshuhudia mvutano mkali kati ya wanasiasa wenye itakadi kali za kidini, walio na msimamo wastani na mawaziri waliotumikia utawala wa aliyekuwa Rais Hosni Mubarak.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapiga kura wengi zaidi watajitokeza leo

Msemaji wa serikali ya Marekani Victoria Nuland amepongeza maandalizi ya uchaguzi huo ambao amesema ni hatua muhimu ya demokrasia nchini Misri.

Wagombea wanaopewa nafasi nzuri kwenye uchaguzi huo ni Ahmed Shafiq, aliyekuwa kamanda wa jeshi la angani na Amr Moussa, aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje na kiongozi wa jumuiya ya nchi za kiarabu.

Wengine ni Mohammed Mursi, kiongozi wa vugu vugu la kiislamu, Muslim Brotherhood na Abdul Moneim Aboul Fotouh, mgombea binafsi lakini ambaye pia anegemea sera za kidini.

Uchaguzi huu utafanyika kwa siku mbili kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura na ikiwa mshindi hatapatikana, duru ya pili ya uchaguzi itafanyika j Juni tarehe 16 na 17.