UN," Zimbabwe iondolewe vikwazo"

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Navi Pillay akiwa Zimbabwe

Kamishina mkuu wa tume ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay amezitaka nchi za magharibi kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Zimbabwe.

Akizungumza kwenye ziara mjini Harare Bi Pillay amesema vikwazo vya sasa vinawuamiza masikini. Aidha ametaka utawala wa Zimbabwe kutekeleza mageuzi muhimu ili kujiepusha na machafuko ya kisiasa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao.

Muungano wa Ulaya tayari umeondoa baadhi ya vikwazo japo umeweka masharti dhidi ya Rais Robert Mugabe na washirika wake.Rais Mugabe pamoja na washirika wake 100 wamezuia kuzuru Ulaya pamoja na mali zao kupigwa tanji.

Uingereza imekuwa ikisisitiza kwamba vikwazo dhidi ya Zimbabwe haziathiri masikini lakini Mkuu wa Haki za Binadamu amepinga kauli hio.

Muungano wa Ulaya uliweka vikwazo dhidi ya Zimbabwe baada ya uchaguzi mkuu wa Zimbabwe mwaka 2008 ambapo wafuasi wa rais Robert Mubage walituhumiwa kwa kuwapiga, kuwatesa na hata kuwaua mamia ya watu.

Mgogoro wa uwongozi ulimlazimu Rais Mugabe kugawana madaraka na mpinzani wake Morgan Tsvangirai ambaye anahudumu kama Waziri Mkuu.

Mapema mwaka huu Shirika la kutetetea haki za binadamu Human Rights Watch liliomba vikwazo hivyo kuendelea hadi pale Zimbabwe itakaporekebisha hali ya kibinadamu.