Sweden bingwa wa Eurovision

Loreen Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mzaliwa Sweden na mwenye asili ya Morocco aliibuka mshindi wa Eurovision

Mwanamuziki aliyetazamiwa kuibuka bingwa katika mashindano ya muziki kwa mataifa ya Ulaya, Loreen kutoka Sweden, kama ilivyofikiriwa, aliibuka mshindi wa mashindano ya 57 ya Eurovision siku ya Jumamosi, akiimba wimbo wake wa dansi, Euphoria.

Loreen aliongoza tangu mwanzo kura zilipoanza kutangazwa, na upinzani wa pekee uliojitokeza ni kutoka kwa bibi vizee wa Urusi, walioshiriki katika mashindano kwa kutumia jina Buranovo Grannies, na wenyeji Azerbaijan.

Kwa mara nyingine tena Uingereza haikufua dafu katika mashindano hayo, na mwanamuziki wake Engelbert Humperdinck, ambaye alifungua mashindano kwa wimbo Love Will Set You Free, alishikilia nafasi ya pili kutoka mwisho.

Hata hivyo mwanamuziki huyo, mwenye umri wa miaka 76, aliepuka fedheha ya kutopata kura zozote.

Engelbert, licha ya kuuza rekodi milioni 150 kote ulimwenguni, alipata jumla ya pointi 12, kutoka mataifa ya Estonia, Latvia, Ubelgiji na Ireland.

Uingereza haijawahi kushinda mashindano hayo tangu mwaka 1997, na mara tatu imekuwa ya mwisho katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Katika historia ya mashindano hayo, hakuna mwanamuziki aliyewahi kufungua mashindano na kuibuka mshindi, kwani watazamaji wengi wa televisheni hupata mashindano yakiwa tayari yameanza, na hukosa kuwaona wanamuziki waliotangulia.

Mataifa 26 yalishiriki katika fainali hizo za Azerbaijan, katika ukumbi wa Crystal, na uliokuwa na wapenda muziki 20,000.

Inakisiwa watu milioni 125 kote ulimwenguni hutizama mashindano hayo kupitia runinga.