Umoja wa Mataifa waishutumu Syria

Milli ya waliouwawa Houla,Syria Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Milli ya waliouwawa Houla, Syria

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu matumizi ya silaha nzito zinazotumiwa na majeshi ya serikali ya Syria dhidi ya raia katika mji wa Houla, ambako zaidi ya watu mia moja wakiwemo watoto waliuawa, Ijumaa iliyopita.

Taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imesema mji huo ulishambuliwa kwa makombora na vifaru, mashambulio ambayo taarifa hiyo imeyataja kuwa ni matumizi mabaya ya nguvu dhidi ya raia ambayo yanakiuka sheria za kimataifa.

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari, amekanusha taarifa hiyo ambayo ameiita kuwa ni tsunami ya uongo unaoenezwa na wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao wanaishutumu serikali yake kutokana na vifo hivyo.

ghasia zaendelea

Ripoti mpya kutoka Syria zinasema ghasia zinaendelea nchini humo.

Wanaharakati wa upinzani nchini Syria wanasema watu wapatao thelathini waliuawa katika mji wa Hama jana, Jumapili, wakati vikosi vya serikali viliposhambulia maeneo kadha ya mji huo ambayo yalitumiwa kama ngome na wapiganaji waasi.

Hata hivyo taarifa hiyo haijaweza kuthibitishwa na upande huru.