Mchoro wa Zuma 'akiwa uchi' waondolewa

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mchoro wa Zuma ukionyesha sehemu zake za siri waondolewa hadharani

Gazeti la moja la Afrika Kusini limeondoa kutoka kwenye wavuti wake picha ya mchoro wenye utata unaoonyesha sehemu za siri za Rais Jacob Zuma zikiwa nje.

Mchoro huo ‘The Spear’ umeondolewa kama hatua ya ‘kuleta moyo wa amani …na hofu pia " mhariri Ferial Haffajee ameandika katika maoni ya Gazeti la City Press.

Chama cha ANC kilitoa wito wa kususiwa kwa gazeti hilo na wiki iliyopita kilikwenda mahakamani kutaka mchoro huo uondolewe hadharani.

Watu wanaopinga mchoro huo waliuharibu.

Mchoro wa ‘The Spear’ uliochorwa na Brett Murray, msanii anayejulikana kwa kazi zake za kisiasa na zenye utata , umezusha moto nchini Afrika Kusini.

Maelfu ya watu wameandamana wakipinga huku wakisema haki ya utu wa Rais Zuma imevunjwa, huku wanaomuunga mkono wakisema huu ni mjadala wa uhuru wa kujieleza na vyote hivi vinalindwa na katiba ya Afrika Kusini.

Kesi ilifunguliwa na chama cha ANC dhidi ya mtandao wa City Press na shirika la Goodman Gallery mjini Johannesburg, ambalo ndilo liliendesha maonyesho ya sanaa, maonyesho hayo yamefungwa kwa muda usiojulikana.

Hata hivyo Bi Haffajee aliamua kuuondoa mchoro huo kwa sababu hali imekuwa ni ya ‘moto’

Mwandishi wa City Press amezuiwa kuripoti habari za mkutano wa shirikisho la wafanyakazi, nakala za gazeti la City Press kuchomwa moto na wahariri na wafanyakazi wengine kutishiwa, Bi Haffajee anasema.

"Kwa ajili ya usalama, kujali na kusaidia hali iwe tulivu nimeamua kuondoa picha hiyo,’ alisema.

"Kwa kuwa sasa tumekuwa ishara ya hasira ya Taifa, kuzusha ghadhabu si wajibu wa vyombo vya habari katika jamii," alisema.