Sudan na Sudan Kusini kuanza mazungumzo

mpatanashi wa mazungumzo ya Sudan, Thambo Mbeki Haki miliki ya picha AFP
Image caption mpatanashi wa mazungumzo ya Sudan, Thambo Mbeki

Sudan na Sudan Kusini leo wanakutana katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya nchi hizo majirani.

Mazungumzo hayo yamekuja kufuatia ushawishi wa kidiplomasia na kitisho kutoka Umoja wa Mataifa kuziwekea vikwazo nchi hizo iwapo zitashindwa kukaa pamoja kujadili mgogoro baina yao.

Mzozo kati ya Sudan na Sudan Kusini ulioibuka mwezi uliopita baada ya Sudan Kusini kushambulia na kudhibiti eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta wa Hijlig, Lakini baadaye kuondoa majeshi yake.

Nchi hizo mbili zinatofautiana kuhusu maswala mbali mbali zikiwemo jinsi ya kugawanya mafuta ya nchi hizo na kuweka mipaka.

ajenda

Jamhuri ya Sudan imesema kuwa lazima swala la usalama lishughulikiwe kabla ya mambo mengine kusuluhishwa.

Hata hivyo Sudan Kusini inasema maswala yote lazima yawe katika ajenda ya mashauriano haya.

Mwandishi wa BBC mjini Khartoum amesema kuwa wapatanishi- wakiongozwa na aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki- wanakibarua kigumu mbele yao.

Jumatatu, Sudan ilisema kuwa iko tayari kuondoa majeshi yake katika eneo linalozozaniwa la Abyei, ambalo ilitwaa mwaka mmoja uliopita.