Mpinzani wa utumwa ashtakiwa Mauritania

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafuasi wa Bw Obeidi

Mwanaharati wa kupinga utumwa nchini Mauritania ameshtakiwa kwa kutishia usalama wa nchi.

Biram Ould Obeidi amepinga utumwa na kero yake ameionyesha kwa kuvichoma vitabu vya kidini hatua iliyozua maandamano jiji kuu la Nouakchott.

Watu wengine sita wa vuguvugu linalopinga utumwa la Initiative for the Resurgence of Abolitionism in Mauritania (IRA-Mauritania) pia wameshtakiwa. Licha ya utumwa kupigwa marufuku nchini Mauritania ukatili huo bado unaendelea.

Bw. Obeidi ambaye ni kizazi cha utumwa aliongoza maandamano kupinga utumwa baada ya sala ya Ijumaa Aprili 28 ambapo alivichoma vitabu kutoka chuo cha masomo ya dini ya Kiisilamu cha Maliki.

Alisema baadhi ya sura ziliunga mkono utumwa lakini baadaye akaomba radhi akisema kitendo chake hakikunuia kuwaudhi waisilamu.

Maurinatia ni jamii yenye mila na tamaduni zilizokita mizizi. Taifa hili limegawanyika kwa misingi ya kirangi ambapo jamii ya Moors asilia ya waberbers na Waarabu waliwatawala na kuwafanya watumwa raia weusi wanaojulikana kana Haranite. Utumwa uliondolewa kisheria mwaka 1981 na mwaka 2007 sheria ikapitishwa kuwafunga jela miaka sita wanaopatikana wakiwafanya wenzao kuwa watumwa. Hata hivyo baadhi ya watu wameendelea na ukatili huu.

Maelfu ya raia waliandamana mjini Nouakchott, kupinga kuchomwa kwa vitabu hivyo vya kidini. Waendesha mashtaka wamesema Bw Obeidi na wenzake sita walichochea maandamano hayo ambayo yanatishia usalama wa nchi.

Wafuasi wa bw Obeidi wamekuwa wakiandamana tangu mwezi jana kushinikiza aachiwe huru wakisema anakandamizwa kutokana na kuikosoa serikali yake kutokana na haki za binadamu.