Majeshi Syria yaagizwa kuondoka mijini

Waasi Syria Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waasi Syria

Kikundi cha waasi nchini Syria cha Free Syrian Army, kimeipatia serikali ya nchi hiyo muda wa saa arobaini na nane kuondoa majeshi yake kutoka miji na vijiji vya nchi hiyo, la sivyo kitaachana na utekelezaji wa mpango wa amani wa kimataifa.

Katika picha ya video iliyotumwa katika mtandao wa internet, afisa mwasi amesema iwapo serikali itashindwa kukubaliana na agizo hilo kufikia kesho mchana kwa saa za Syria, hakutakuwa na sababu tena kwa wapiganaji waasi peke yao kuwataka kusitisha mapigano.

baraza la usalama

Mapema, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lilipata taarifa kuwa isingekuwa rahisi kwa serikali ya Syria na waasi kuwa na mazungumzo huku ghasia zikiendelea.

Naibu mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mpango wa amani nchini Syria, Jean Marie Guehenno, amesema upinzani umeacha kuogopa nguvu ya serikali.

Hatahivy, amesema ni muhimu kwa pande zote zinazohusika na mgogoro nchini humo kukubaliana na hatua ya kusitisha mapigano, kwa sababu kinyume chake, vita vya wenyewe kwa wenyewe vitakapozuka nchini Syria hali itakuwa mbaya zaidi.