Assad asema Syria yakabili vita halisi

Rais Assad ameliambia bunge la Syria kwamba nchi inakabili uhasama wa nchi jirani na kimataifa.

Haki miliki ya picha AP

Alisema kunafanywa jaribio la kuidhoofisha Syria, ambayo inakabili kipindi kibaya kabisa katika historia yake tangu ukoloni kumalizika.

Lakini alisema Syria itaendelea na mpango wake wa kuleta mabadiliko, ili kuwajumuisha wananchi zaidi kwenye siasa.

Rais Assad alisema hakuna njia ya kuukimbia msukosuko , lakini kuukabili piya kutaumiza.

Alisema ugaidi unazidi nchini Syria.

Ni lazima kuuzuwia kabla ya mabadiliko ya kisiasa kuendelea, kwani watu wanaofanya ugaidi hawana hamu ya mazungumzo.

Alisema Syria inakabili vita halisi, lakini watu wamekataa jumuia ya kimataifa kuingilia kati ya mambo ya ndani ya nchi yao.

Rais Assad alisema mlango ungali wazi kwa wale wanaotaka mazungumzo kutoka upande wowote wa upinzani.

Lakini siyo wale wanaoshiriki katika vitendo vya kigaidi, au wanafuata amri za mataifa ya kigeni.