Ripoti yasema Rwanda inaunga uasi DRC

Haki miliki ya picha
Image caption Waasi Mashariki mwa DRC

Ushahidi mpya unaonyesha kwamba jeshi la Rwanda linawasaidia waasi katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch.Shirika hilo limesema waasi wa zamani wameelezea jinsi Rwanda iliwasajili wapiganaji kujiunga na waasi pamoja na kutoa silaha.

Rwanda pia imedaiwa kutoa hifadhi kwa Jenerali muasi Bosco Ntaganda,anayetakikana na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC. Serikali ya Rwanda imekanusa kuwafadhili waasi hao.

Waandishi wa habari wamesema japo ripoti hii haijailaumu moja kwa moja serikali ya Rwanda kwa kuwafadhili waasi, hata hivyo imeutaka utawala wa Kigali kuhakikisha vitendo vya kuwasajili wapiganaji na kuvukisha silaha vinadhibitiwa.

Maasi yanayoendelea Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanaongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda, ambaye zamani alikuwa kamanda katika kundi la waasi wa CNDP lakini baadaye lilijumuishwa katika jeshi la Congo mwaka 2009 kufuatia mkataba wa amani.