Mamluki Liberia watumia watoto vitani

Shirika la haki za binadamu lenye makao yake mjini New York, Human Rights Watch, linasema kua wanamgambo wanaoipinga serikali ya Ivory Coast wameandika askari watoto kutoka Liberia na kufanya mashambulio baada ya kuvuka mpaka.

Image caption Rais wa Ivory Coast

Shirika hilo linasema kua wapiganaji hao waliwalenga wafuasi wa Rais Alassane Ouattara, na kua takriban watu 40 waliuawa.

Washambuliaji wanasemekana kua raia wa Ivory Coast wakishirikiana na wa Liberia waliokua wapiganaji wa Rais wa zamani wa nchi hio, Laurent Gbagbo.

Human Rights Watch linasema kua mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu 40 kwa uchache tangu mwezi julai mwaka 2011.

Mamiya ya askari mamluki kutoka Liberia walishiriki vita kwa niaba ya Rais aliyepinduliwa Ivory Coast Laurent Gbagbo katika machafuko ya mwaka jana.

Wakiwa pamoja na raia wa Ivory Coast wengi walivuka mpaka na kukimbilia Liberia.

Katika taarifa, Shirika hilo linasema kua wapiganaji hao wanaandika watoto wenye umri mdogo wa hadi miaka 14 kuvamia raia wa Ivory Coast wanaomuunga mkono Rais wa sasa wa Ivory Coast, Alassane Ouattara na wanaoishi karibu na mpaka.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Laurent Gbagbo

Mwezi Julai mwaka jana kitendo cha Bw.Gbagbo cha kukataa kuachia madaraka baada ya uchaguzi wa Disemba mwaka 2012 kulisababisha ghasia.

Hatimaye Bw.Gbagbo alikamatwa na kukabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa (ICC) kukabili tuhuma za uhalifu dhidi ya Binadamu.

Mamiya ya mamluki wa Liberia pamoja na wakereketwa wa Ivory Coast waliopigana kwa niaba ya Bw. Gbagbo hivi sasa wanaishi nchini Liberia na hawajafikishwa mbele ya vyombo vya sheria mjini Monrovia huko Liberia.

Taarifa ya Human Rights watch ilifanywa kwa upelelezi uliofanywa katika miji ya Liberia iliyo karibu na mpaka wa Ivory Coast.

Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 17 aliyehojiwa katika taarifa ya shirika hilo alikiri kuongoza watoto wenzake katika shambulio la kuvuka mpaka.

Watu wengine waliohojiwa walisema kua waliwaona watoto wenye umri ulio kati ya miaka 14 na 17 ndani ya kambi za mafunzo ya kijeshi.

Taarifa hii inahimiza hofu ya Umoja wa Mataifa kwamba serikali ya Liberia haijachukua hatua zinazostahiki dhidi ya mamluki wa Liberia na wenzao wa Ivory Coast wanaotuhumiwa kwa uhalifu katika vita.