Wapiganaji wa Ivory Coast wasakwa

Naibu waziri wa ulinzi wa Ivory Coast anasema kuwa serikali na Umoja wa Mataifa, watafanya operesheni ya pamoja Jumatatu, kuwasaka wale waliohusika na shambulio la Ijumaa dhidi ya askari wa Umoja wa Mataifa, na kuwauwa askari 7 pamoja na raia.

Haki miliki ya picha AP

Paul Koffi alisema washambuliaji walikuwa wapiganaji au askari mamluki ambao wamepata mafunzo nchi ya jirani, Liberia.

Serikali ya Ivory Coast inasema wanajeshi na raia wake kadha waliuwawa piya Ijumaa, katika shambulio la kuvizia, ambalo lilikuwa la kwanza la aina hiyo, na ambalo lililenga hasa kikosi cha usalama cha Umoja wa Mataifa.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha jumla ya askari elfu 16, kimezidisha ulinzi pande zote mbili za mpaka baina ya Ivory Coast na Liberia.

Wapiganaji wa rais wa zamani, Laurent Gbagbo walikimbilia Liberia baada ya kiongozi wao kukamatwa, katika ghasia zilizozuka wakati wa uchaguzi wa rais wa mwaka jana.

Wakuu wa Ivory Coast sasa wanasema watawasaka wapiganaji hao waliouwa askari wa Umoja wa Mataifa, lakini hawawezi kufanya hivyo bila ya msaada wa wakuu wa Liberia; ambao juma hili wameshutumiwa na mashirika ya haki za kibinaadamu, kwamba wanawafungia macho wapiganaji walioko kwenye ardhi yao.