Raia Eritrea akiri kusaidia al-shabab

Imebadilishwa: 14 Juni, 2012 - Saa 12:05 GMT

Baadhi ya wapiganaji wa kundi al-Shabab

Raia waEritrea amekiri mahakamani nchini Marekani kupewa mafunzo ya kijeshi kutoka kwa kundi la wapiganaji wa al-Shaban.

Mohamed Ibrahim Ahmed, mkazi wa Sweden, alikwenda Somalia mwaka 2009 kujifunza kutengeneza mabomu na ujuzi wa kuyalipua, wakili wa serikali alisema.

Pia alichangia euro 3,000 ($3,769, £2,433) kwa wapiganaji wa Kiislam, nyaraka za mahakama zilionyesha.

Al-Shabab, lililojiunga na al-Qaeda mapema mwaka huu linapigana na serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 38 anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani na hukumu yake itasomwa mwezi Novemba.

Ahmed alikamatwa Nigeria mwaka 2009 na kuhamishiwa mahabusu Marekani miezi minne baadaye.

"Mohamed Ibrahim Ahmed alisafiri kutoka anakoishi Sweden hadi Somalia, ambako alichukua mwelekeo wa al-Shabab, kundi hatari la kigaidi na kuapishwa kuwa adui wa Marekani na watu wake. " Wakili wa Manhattan Pree Bharara alisema katika taarifa.

Kwa mujibu wa nyaraka za Mahakama, akiwa Somalia aliweza pia kununua bunduki aina ya AK-47, kuongeza ‘magazine’ na maguruneti mawili.

Silaha na risasi zake hatimaye alipewa kamanda wa al-Shabab.

Al-Shabab linajulikana kusajili idadi kadhaa ya wapiganaji wa kigeni wengi wakiwa wamepigana nchini Iraq na Afghanistan.

Wiki iliyopita serikali ya Marekani ilitangaza ofa ya mamilioni ya dola kama zawadi kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa viongozi saba wa al-Shabab.

Miongoni mwa waliokuwa wakitafutwa ni Mswisi mwenye asili ya Kisomali Fuad Mohamed Khalaf, anayejulikana pia kama Shongole, anayefadhili kundi hilo.

Somalia haina serikali thabiti tangu mwaka 1991, na imekumbwa na mapigano tangu wakati huo hali ambayo imesababisha uharamia na kukosekana kwa utawala kisheria kuongezeka.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.