Misri:maandamano makubwa kupinga jeshi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Muslim Brotherhood wapinga Jeshi kujilimbikizia madaraka

Wafuasi wa Muslim Brotherhood watafanya maandamano makubwa kote nchini Misri kupinga hatua ya baraza la kijeshi la nchi hiyo kujilimbikizia madaraka.

Mwishoni mwa wiki iliyopita wakuu wa jeshi la Misri walitangaza amri ya kuvunjwa kwa bunge na halafu kijitwika madaraka ya bunge hilo.

Hii leo Jumanne wabunge ambao wengi wao ni wafuasi wa Muslim Brotherhood wanatarajiwa kujaribu kuingia bungeni kwa nguvu.

Na wakati kura za urais zingali zinahesabiwa,wagumbezi wote wawili wamedai kupata ushindi.

Mohammed Mursi, ambae ni kiongozi wa chama cha Brotherhood's Freedom and Justice Party (FJP), siku ya jumatatu alitangaza kwamba amepata jumla ya asilimia 52 ya kura zilizopigwa siku ya Jumapili.

Bwana Mursi aliahidi kushirikiana na Wa-Misri wote kuhakikisha kuna maisha bora, uhuru zaidi, demokrasia na amani imedumishwa kote nchini.

Lakini wasimamizi wa kampeni ya Bwana Ahmed Shafiq ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa mwisho wa Misri amedai kuwa yeye ndie mshindi wa kura hizo na wafuasi wa Muslim Brotherhood waliwatisha wapiga kura.

Hata hivyo vyombo vya habari vya kitaifa pamoja na waangalizi huru wa kura hizo wanaamini kuwa Bwana Mursi ameshinda uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia tatu au nne ambayo ni zaidi ya kura milioni moja.

Inaonekana kwamba baraza kuu la kijeshi la Misri linaamini kwamba Bwana Mursi ndie ataibuka mshinda hivyo basi ikatangaza amri ya kupunguza uwezo na mamlaka ya rais.