Rubani wa Syria atua Jordan

Ndege kijeshi imetua kwenye kituo cha majeshi kilichoko kaskazini mwa Jordan na rubani kuomba hifadhi, wamesema wakuu wa Jordan.

Image caption Ndege MiG21

Waziri wa Habari wa Jordan Samih al-Maaytah amesema kua rubani wa ndege aina ya MiG 21 alikua akihojiwa.

Runinga ya Syria imetangaza katika taarifa zake za habari kua ndege moja ya kijeshi iliyokua ikiendeshwa na rubani wa ngazi ya Kanali ilipotea wakati wa mazowezi.

Tukio hili linakuja wakati mji wa Homs unashambuliwa kwa makombora na makundi ya wahudumu wa msalaba mwekundu wakisubiri kuingia ili kuwanusuru raia.

Ndege hiyo muundo wa MiG 21 iliyoundwa Urussi ilitua kwenye kambi ya jeshi la anga ya Mfalme Hussein huko Mafraq, karibu mno na mpaka wa nchi hio na Syria.

Inaaminika kua hili ni tukio la kwanza kwa rubani wa Syria kuitoroka nchi yake akiwa na ndege yake.

Msemaji wa kundi la waasi la ''Free Syrian Army,'' Ahmad Kassem, amesema kua kundi hilo limekua likimshinikiza rubani huyo alikimbie jeshi la Syria.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mpiganaji wa waasi

Shirika la habari la Syria, Sana limemtaja rubani huyo kama Kanali Hassan Mirei al-Hamadeh, na kuongezea kua ndege yake ilikua ikiruka karibu na mpaka wa kusini wakati mawasiliano yalipotoweka mwendo wa saa nne na nusu asubuhi.

Duru za usalama nchini Jordan zimesema kua rubani huyo alitoka uwanja wa kijeshi wa al-Dumair, ulio kaskazini mashariki mwa Damascus.

Mashambulio ya makombora makali

Huko Homs, vikosi vya serikali na wapiganaji waasi waliafikiana siku ya jumatano kusitisha mapigano kwa mda wa saa mbili ili kuwawezesha wafanyikazi wa mashirika ya misaada kuingia katika maeneo yaliyoathirika mno na mapigano.

Shirika la Kimataifa la msalaba mwekundu(ICRC), kwa ushirikiano na tawi la mwezi mwekundu la Kiarabu la Syria yameandaa makundi ya wahudumu tayari kwa shughuli ya kuwaondoa raia, ingawa mashambulio yanaendelea.

Mkaazi wa eneo moja ambako ICRC inataka kuingia, Waleed Faris, amesema kua mashambulio hayo yalikua makali mno majira ya alfajiri lakini yalipungua baadaye.

Mwandishi wa BBC Jim Muir mjini Beirut anasema yumkini kuna masuala kadha wa kadha ambayo yamechangia kucheleesha shughuli ya uokozi, mfano ni jinsi gani magari yataruhusiwa kuingia na kutoka na majeruhi watapelekwa wapi ili wapewe matibabu. Hilo linaweza kufanyika baada ya saa nyingi, au hata siku kusuluhisha, anasema mwandishi huyo.