Wakuu wa Mafuta Nigeria wafutwa kazi

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Maandamano kupinga kuondolewa ruzuku ya mafuta Nigeria

Rais wa Nigeria GoodLuck Jonathan amemuachisha kazi mkurugenzi mkuu na maafisa kadhaa wa juu katika wa shirika la mafuta nchini NNPC.

Taarifa kutoka afisi ya Rais imesema hatua ya sasa imechukuliwa kwa ili kuhakikisha kuwepo uwajibikaji miongoni mwa maafisa wa umma.

Nigeria ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi lakini taifa hilo limekumbwa na visa vingi vya ufisadi.

Ripoti ya karibuni iliyotayarishwa na bunge ilisema dola bilioni 6.8 zimefujwa. Kamati ya kuchunguza sekta ya mafuta ilibuniwa kufuatia mgomo wa kiaifa mapema mwaka huu baada ya serikali kuondoa ruzuku inayoweka kwa bei ya mafuta.

Raslimali ya mafuta huchangia asili mia 80 ya mapato ya Nigeria lakini nchi hiyo haijaweza kusafisha mafuta, na hivyo hulazimika kuagiza mafuta safi kutoka nje.

Ripoti ya kamati ya bunge imesema ubadhirifu wa fedha na biashara za magendo ndani ya shirika hilo la mafuta nchini.

Japo japo serikali hutoa ruzuku kwa lita milioni 59 za mafuta kwa siku wateja wa Nigeria kupokea lita milioni 35 za mafuta pekee.

Mkurugenzi Mkuu wa NNPC Austen Oniwon ameondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Andrew Yakubu.

Mnamo mwezi Februari mkuu wa zamani wa tume ya kukabiliana na ufisadi Nuhu Ribadu aliteuliwa kuongoza jopo maalum kuchunguza usimamizi wa fedha za umma katika sekta ya mafuta pamoja na kutathmini uzalishaji wa mafuta na mauzo yake nje ya nchi.