El-Bashir atimiza miaka 23 ya uongozi

Miaka 23 iliyopita, mwanajeshi mmoja asiyejulikana sana, alifanya mapinduzi na kunyakua madaraka nchini Sudan. Tangu wakati huo, Omar el Bashir ameongoza nchi, juu ya vita vya Darfur na Sudan Kusini kujitenga na kuwa nchi huru.

Lakini sasa anakabili matatizo mengi.

Wakati wake wote wa uongozi, Rais Omar el Bashir, hakupata kuona amani nchini mwake.

Wakati vita virefu vya kusini vilipoanza kupungua miaka 10 iliyopita, vita vengine vilizuka Darfur, magharibi mwa Sudan.

Mwaka wa 2005 Rais Bashir alitia saini mkataba wa amani na wapiganaji wa kusini, ambao baadae ulipelekea Sudan Kusini kujitenga na kuwa huru.

Lakini vita vya Darfur vinaendelea.

Rais Bashir ameshtakiwa na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa, ICC, kwa mauaji yaliyotokea Darfur.

Na sasa anakabili vita kwenye majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile.

Uchumi umeporomoka baada ya Sudan Kusini kumnyima mapato ya mafuta.

Katika majuma mawili yaliyopita, kumefanywa maandamano kadha, kupinga hatua kali za kiuchumi, na kulalamika juu ya Rais Bashir mwenyewe.