GlaxoSmithKline kulipa faini ya $3b

Dawa ya Wellbutrin Haki miliki ya picha Getty
Image caption Dawa ya Wellbutrin

Mojawapo wa kampuni kubwa zaidi duniani ya dawa, GlaxoSmithKline, imekubali kulipa faini ya $3b katika sakata ambayo imetajwa kuwa ulaghai mkubwa zaidi kuwahi kukumba sekta ya afya katika historia ya Marekani.

Kampuni hiyo ya GlaxoSmithKline, inashutumiwa kuvunja sheria za Marekani kuhusiana na jinsi ilivyouza bidhaa zake mbali mbali.

Miongoni mwa madai yanayokabili kampuni ya GSK ni kuwa kampuni hiyo ilijaribu kuwashawishi wagonjwa walio chini ya umri wa miaka 18 kutumia madawa ya dawa ya kupunguza simanzi, Paxil, ambaylo ilikuwa imeidhinishwa kwa watu wazima wanaozidi umri huo pekee.

Naibu wa Mwanasheria Mkuu nchini Marekani, James Cole aliwambia waandishi wa habari mjini Washington kuwa kesi hiyo ni ya aina ya kipekee. Amesema malipo hayo ndiyo makubwa zaidi kuwahi kutolewa kama faini katika historia ya huduma za afya katika historia ya Marekani'.

Naibu huyo wa mwanasheria mkuu huyo alisema kuwa kuna ushahidi kwamba kampuni hiyo ilijaribu kuwanunulia madaktari vyakula na anasa zingine, ambazo zinaweza kutambuliwa kama hongo ili watumie madawa ambayo hayakuwa yameidhinishwa.

Kampuni hiyo pia ililaumiwa kwa kutanganza matumizi ya dawa nyingine, Wellbutrin, kwa matumizi ambayo hayakuwa yameidhinishwa.

Kampuni hiyo imetoa taarifa na kusema kuwa haitarudia kosa hilo kwani imejifunza kutokana na makosa ya sasa.