Barabara yafunguliwa tena Pakistan

Magari ya kusafirisha bidhaa za NATO Haki miliki ya picha AP
Image caption Magari ya kusafirisha bidhaa za NATO

Serikali ya Pakistan imesema itafungua upya barabara zinazotumiwa kusafirishia bidhaa za wanajeshi wa muungano wa NATO nchini Afghanistan.

Hii ni baada ya kupokea rasmi ombi la msamaha kutoka kwa serikali ya Marekani, kufuatia mashambulio ya anga yaliyotekelezwa na wanajeshi wa marekani, yaliyopelekea kuuawa kwa wanajeshji ishirini na wanne wa nchini Hiyo.

Waziri wa mambo ya nje wa marekani, Bi Hillary Clinton, amesema serikali ya Pakistan imeamua kufungua upya barabara hizo zinazotumiwa kusafirisha bidhaa za wanajeshi wa muungano wa NATO, ambazo zilifungwa mwezi Novemba mwaka uliopita.

Pakistan ilifunga barabara hizo baada ya wanajeshi 24 wake kuuawa kwenye shambulio la anga lililotekelezwa na wanajeshi wa muungano wa NATO.

Bi Clinton ameafiki tangazo hilo na kuomba radhi kufuatia shambulio hilo.

Amesema amefahamishwa na waziri wa mambo ya nje wa Pakistan kuwa barabara hizo zinafunguliwa tena.

Bi Clinton, amesema serikali ya Pakistan haitatoza ushuru zaidi bidhaa zitakazosafirishwa kupitia nchi hiyo.

Waziri mkuu wa Pakistan, Raja Pervez Ashraf amesema ufunguzi tena wa barabara hizo muhimu utasaidia kuimarisha uhusiano kati ya Pakistan na Marekani na pia ni mchango wa serikali yake ya kuafikiwa kwa hali ya uthabiti na usalama katika nchi jirani ya Afghanistan.