Tume ya Uchaguzi Libya yakiri mapungufu

Kituo cha kupigia kura Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kituo cha kupigia kura

Wananchi wa Libya wanapiga kura katika uchaguzi wao wa mwanzo wa taifa kwa karibu nusu karne.

Wanasiasa zaidi ya elfu-3 wanagombea viti katika bunge jipya, ambalo litachukua nafasi ya Halmashauri ya Mpito ya Taifa iliyoundwa baada ya Kanali Muammar Gaddafi, kuondolewa madarakani, miezi tisa iliyopita. Bunge litateua serikali ya muda na kutayarisha katiba mpya.

Kikundi cha wanawake mjini Tripoli kilifurahi na kupiga vigelegele wakati wa kupiga kura.

Wapigaji kura katika mji mkuu, walisema uchaguzi huo ni tukio muhimu kwa nchi yao. Huyu mmoja alisema leo ni siku ya furaha.

"Najihisi kama bwana harusi. Ni kama sherehe ya harusi, harusi ya demokrasi leo. Hii ni mara yetu ya kwanza, tunachagua nani atatuongoza, na watu wanajihisi uzuri. Tunashukuru Mungu.")

Mwandishi wa BBC anasema uchaguzi huo unafanywa wakati machafuko yanazidi mashariki mwa Libya, kwa sababu baadhi ya makundi yanaona hayatawakilishwa vya kutosha.

Upigaji kura kwenye miji miwili ya masharikii umesimamishwa, baada ya karatasi za kura kuibiwa pamoja na mihuri.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mkuu wa tume ya uchaguzi Nuri al Abar

Mjini Benghazi, kituo cha kupigia kura kilifyatuliwa risasi, na zana zote za uchaguzi ziliharibiwa.

Uchaguzi huu hata hivyo ulitanguliwa na ghasia pamoja na ukabila. Mfanyikazi mmoja wa tume ya uchaguzi aliuawa kwenye mkesha wa kupiga kura baada ya watu wenye silaha kushambulia helikopta karibu na mji wa Benghazi.

Watu wengi wa mashariki mwa nchi wana wasiwasi kuwa eneo lao lenye utajiri mkubwa wa mafuta halitokua na wawakilishi wa kutosha katika bunge.

Wakuu wa Uchaguzi wamekiri kuwa kweli shughuli ya uchaguzi zimekuwa na mapungufu mengi lakini ilikua muhimu kuendelea na shughuli hiyo.