Bunge Misri larejelea vikao kwa muda

Bunge La Misri Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bunge La Misri

Bunge la Misri limerejelea vikao vyake mapema hii leo kufuatia agizo lililotolewa na rais mpya wa nchi hiyo Mohamed Mosri, lakini kikao hicho kikaahirishwa baada ya muda mfupi.

Bunge hilo lilirejelea vikao vyake na kukiuka agizo lililotolewa na Baraza la Kijeshi linalotawala, ambalo lilivunja bunge hilo kufuatia uamuzi wa mahakama ya kikatiba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, mapema hii leo, Baraza hilo la Kijeshi lilisema kuwa ni sharti raia wote wa nchi hiyo waheshimu uamuzi uliotolewa na mahakama ya kikatiba.

Mwandishi wa BBC mjini Cairo, anasema malumbano makali yanaendelea kutokota kati ya rais Morsi na maafisa waandamizi wa jeshi. Hata hivyo rais Morsi alijitokeza hiyo jana katika hafla rasmi ya serikali akiandamana na maafisa kadhaa waandamizi wa Baraza hilo la Kijeshi.