Mahakama yapindua amri ya Mursi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Mursi aliagiza bunge lianze tena vikao vyake

Mahakama ya juu zaidi nchini Misri imepindua amri ya Rais Mohammed Mursi ya kuagiza bunge lianze vikao vyake.

Rais Mursi alikuwa amepuuza hatua ya baraza kuu la kijeshi la kuvunja bunge.

Wabunge walikutana kwa muda mfupi kabla ya mahakama ya juu zaidi kutoa agizo lake jipya.

Na maelfu wa watu wamekusanyika katika medani ya Taharir kupinga uamuzi wa mahakama hiyo ya juu.

Waandamanaji wamekuwa wakipiga kelele wakisema hatua hiyo ni haramu na pia kulilaani baraza la kijeshi la Misri.

Mwandishi wa BBC mjini Cairo Jon Leyne anasema kuamuzi wa mahakama hiyo umeleta hali ya utata kuhusu ni nani hasa ana uwezo na majukumu ambayo kawaida hutekelezwa na bunge la nchi.

Kuna dalili kwamba kitakachofuata sasa ni vita vya kisheria vya muda mrefu kuhusu nani mwenye mamlaka halisi.

Kwa sasa huenda rais na jeshi wakjaanza kushindani kila mmoja aktika kuonyesha kuwa na uwezo zaidi.

Na kuna hofu kuwa maandamano huenda yakaanza tena nchini Misri.

Katika bunge ambalo Mahakama ya juu zaidi ili agiza livyunjwe wengi ya wabunge walikuwa ni wanachama wa Muslim Brotherhood.

Siku ya Jumanne wabunge waliitikia amri ya Rais Mursi na kukutana kwa muda mfupi kabla ya vikao vyake kuhairishwa tena na Spika Saada al-Katatni.