Idadi ya wakimbizi yaongezeka Daadab

Idadi inaongezeka
Image caption Kambi ya Daadab mashakani

Idadi ya watu wanaokimbilia kwenye kambi ya wakimbizi ya Dadaab imeongezeka na kufikia watu laki nne na elfu sitini na tano. Mashirika yanayotoa misaada yameonya kuwa kati ya idadi hiyo, takriban watu laki moja na elfu thalathini watakosa makaazi hivi karibuni na kuishi katika mazingira magumu ndani ya hema zisizoweza kuhimili dhoruba ya upepo na mvua.

Msemaji wa shirika la Oxfam ameiambia BBC kuwa wakimbizi waliowasili kambini hivi karibuni hawana vifaa vyovyote, ila wanategemea mifuko ya plastiki na karatasi za maboksi na matawi ya miti.

Image caption Kambi imefurika wakimbizi

Mashirika yameonya kuwa kuanzia mwezi septemba kutakuwa na upungufu wa maji na vyoo halikadhalika huduma za afya. Kwa wakati huu wahudumu wa afya wamezidiwa na idadi kubwa ya watu -mfano uliopo wa vituo viwili vya afya katika kambi ya Hagadera inayohudumia wakimbizi 78,000.

Wakati vyombo vya habari vikizingatia kuwa kiwango cha wakimbizi wanaoingia kambini kinaliongana na mchango wa pesa zilizochangishwa, mtazamo umegeuka na wahisani kubadili maoni yao kuelekea kwingine kama janga la ukame uliolikumba eneo la Sahel.