Kutafuta kiongozi wa AU hakutagawa bara

Mkutano wa kila miezi sita wa viongozi wa Umoja wa Afrika umeanza mjini Addis Ababa.

Haki miliki ya picha

Inatarajiwa kuwa swala muhimu ni kujaribu kumaliza mkwamo katika uchaguzi wa kiongozi mpya wa umoja huo.

Kati ya wagombea wawili - yaani Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma kutoka Afrika Kusini, na mkuu wa sasa, Jean Ping, kutoka Gabon, hakuna aliyeungwa mkono vya kutosha kwenye mkutano uliofanywa Januari, lakini wanagombea tena.

Bibi Dlamini-Zuma alizima wasiwasi kuwa uchaguzi huo utaligawa bara.

"Mimi sifikiri kuwa bara la Afrika litagawika kwa sababu ya kura hii.

Yeyote yule atayechaguliwa, atahakikisha kuwa anaanza kazi yake, anashirikiana na kila mtu, bila ya kujali nani kampigia kura.

Mimi sioni kuwa tatizo kubwa litaloleta mgawanyiko barani Afrika.

Nafikiri tunatia chumvi kulifanya kuwa jambo kubwa."

Waandishi wa habari wanasema mashindano hayo yamechukua muda wa mikutano, ambao ungelifaa kutazama maswala mazito, kama mzozo wa Mali na mvutano baina ya Sudan na Sudan Kusini.