China kukopesha Afrika mabilioni ya dola

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Hu Jintao

Rais Hu Jintao, has wa Uchina ameziahidi serikali za Afrika mkopo wa kadri ya dola za Marekani bilioni 20 kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Amesema kuwa mkopo huo utasaidia katika ujenzi wa miundo mbinu, kilimo na maendeleo ya biashara.

Rais Hu aliyasema hayo wakati wa mkutano wa ushirikiano baina ya Uchina na viongozi wa Afrika mjini Beijing.

Ukianzia barabara mpya za mjini Nairobi hadi wauza kuku katika soko la nchini Zambia ni dhahiri kwamba Uchina imeweka nyayo zake katika kuinua uchumi wa Mataifa mengi barani Afrika.

Miundo mbinu ni mojapo ya sehemu ambazo Uchina imewekeza vilivyo barani Afrika. Biashara kati ya Bara Afrika na Uchina imeongezeka kutoka dola bilioni 10 miaka kumi iliyopita na kufikia takriban dola bilioni mia moja na sitini hii leo. Nchi hiyo imetoa mikopo zaidi kuliko Benki ya Dunia.

Baadhi ya viongozi wa mataifa ya Afrika wamefurahia uhusiano huu wakisema kuwa utakomesha tabia na hali ya kukaliwa na Mataifa ya magharibi kiuchumi na kisiasa kwa masharti yanayokuja na mikopo hiyo.

Kwa upande mwingine Uchina imeshutumiwa na nchi za magharibi kama yenye tamaa, hali inayoifanya kupuuza haki za utu na kupendelea maendeleo ya kiuchumi na mahitaji yake ya nishati.#

Mataifa ya magharibi hayajasita kuinyooshea kidole Uchina kama Mkoloni mpya wa Afrika, kwa kutangaza rekodi yake ya ukiukaji wa haki za binadamu kwa kisingizio cha kuitojiingiza katika masuala ya ndani ya nchi wanakoendesha shughuli zao.

Mfano uliopo ni nchini Sudan ambako mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekosoa uhusiano na Uchina, licha ya vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea huko Darfur. Mashirika hayo yanaongezea kusema kuwa Uchina imesaidia katika kuchochea ghasia kupitia msaada wake wa fedha, silaha na sera.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Viongozi wa Afrika kwenye mkutano China

Kwa upande wake Uchina imesisitiza kuwa itaendelea na sera yake ya kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Mpango wa Uchina kwa Afrika ni bayana. Ina hamu ya mali asili kutoka Bara hilo pamoja na soko la bidhaa zinazotengenezwa Uchina. Vilevile, Uchina inataka kudhibiti ushawishi wake wa kibalozi ulimwenguni kwa msaada wa Afrika.

Hiyo ndiyo hali ilivyo kuhusu miradi ya Uchina kwa Afrika ambapo watu wengi kudhani kuwa Uchina ndiyo inayodhamini miradi yote.

Benki ya Maendeleo ya Afrika, ADB huenda ikahisi kuwa Wachina wameipokonya hadhi yake kutokana na kwamba watu wengi wanaonelea hata miradi ya Benki hiyo na kudhani imedhaminiwa na Wachina, ingawaje fedha zimetoka kwenye Benki hiyo lakini wahandisi na wajenzi ni Wachina.

Viongozi wa Kiafrika hukumbushwa kuhusu mshirika wao mpya wanapokwenda Addis Ababa kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika.

Jengo kabambe la kisasa lililojengwa kwa glasi na mawe kwa gharama ya dfola milioni 200 lilidhaminiwa na Uchina, bila shaka.