Hofu yatanda Syria

Generali Assef Shawkat Haki miliki ya picha AFP
Image caption Generali Assef Shawkat

Mjini Damascus uvumi unasambaa kila mahali lakini jambo ambalo wengi wanaonekana kukubaliana nalo kwa kauli moja ni kwamba, utawala wa rais Beshar Al-Assad, kwa hivi sasa unakabiliwa na tisho kubwa zaidi la kuangamia kuliko wakati mwingine wowote.

Sio kusema kwamba utawala wa Al-Assad unaweza kukatika hivi sasa, lakini kuuawa kwa Assef Shawkat, shemejiye Rais Assad, ni pigo kubwa kwa familia inayotawala.

Yeye ni mtu wa karibu sana kwa rais kuuawa katika machafuko nchini humo na uthibiti na uongozi aliokuwa amejenga katika jeshi sasa umesambaratika.

Kuuawa kwa shemejiye Rais bila shaka kumewafanya watu wengine walioa karibu na kiongozi huyo sasa kuanza kujiuliza ikiwa kweli wako salama sehemu yo yote nchini humo.

Hata hivyo kuna uvumi zaidi kuhusiana na kuuawa kwa Shawkat.

Kuna wale wanaodai kuwa Shawkat aliuawa kwa kupewa sumu siku chache zilizopita na kwamba huenda Waziri wa ulinzi, Daoud Rajha, aliuliwa na serikali yenyewe iliyomshuku kuwa na njama ya kuipindua.

Hakuna ushahidi katiika uvumi huu wote lakini ukweli ni kwamba hakuna ye yote sasa anayeelewa kikamilifu kinachoendelea nchini humo.

Ni vigumu sana kwa waandishi wa habari kutoa taarifa kuhusu yanayoendelea kwa sababu shughuli za uandishi wa habari zimedumazwa na ukosefu wa usalama.

Kuna madai yanayohitilafiana kuhusu nani aliyetekeleza mashambulizi yaliyosababisha mauaji ya vigogo Serikalini huku kundi la waasi la Free Syria Army na kundi lingine dogo la wapiganaji lijulikanalo kama "liwa Al Islamu" kudai kuhusiana na utekelezaji wa shambulio hilo.

Hata njia iliyotumiwa kwa shambulio hilo la mwuaji wa kujitolea mhanga, ambao ni mtindo unaotumiwa hasa na kundei la kigaidi la Al-Qaida, umetia wasiwasi mataifa ya Magharibi pamoja na Urusi.

Wanakubaliana kwa kauli moja kuwa hali nchini syria inafikia mahali ambapo ni pagumu kuthibitiwa.