Selebi wa Afika Kusini kuachiliwa huru

Haki miliki ya picha online
Image caption Jackie Selebi mkuu wa zamani wa polisi Afrika Kusini

Mkuu wa Polisi wa zamani Afrika Kusini Jackie Selebi anatarajiwa kuachiliwa mapema kwenye kifungo chake cha miaka 15 kutokana na rushwa kwa sababu za kiafya, waziri alisema.

Selebi, aliyekuwa kiongozi wa Interpol anahitaji matibabu baada ya figo yake kushindwa kufanya kazi, alisema Waziri wa Huduma za Kurekebisha Tabia, Sibusiso Ndebele.

Alifungwa mwaka 2010 baada ya kukutwa na hatia ya kuchukua hongo kutoka kwa mfanyabiashara wa dawa za kulevya.

Mtangulizi wake Selebi pia alisimamishwa kazi mwaka uliopita kwa tuhuma za rushwa.

Wote Jenerali Bheki Cele na Selebi ni viongozi waandamizi wa Chama Tawala cha ANC.

Selebi, mwenye umri wa miaka 62, alianza kutumia kifungo chake Disemba 2011 baada ya rufaa yake kukataliwa.

Alizirai nyumbani kwake wakati akiangalia televisheni huku Mahakama Kuu ikitoa hukumy yake, na kupelekwa hospitali.

Bodi ya Parole kuhusu afya iliamua mwezi Juni mwaka huu kuwa Selebi aachiliwe huru, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Afrika Kusini.

"Kitengo kina uwezo mdogowa kutoa huduma ya uangalizi wa karibu," Bw Ndebele alisema.

Selebi alihukumiwa kwa kupokea hongo ya randi 1.2m ($156,000; £103,000) kutoka kwa muuza dawa za kulevya Glenn Agliotti ili afumbue macho biashara yake.

Wakati wa kesi yake Mahakama ilisikiliza jinsi Selebi alivyotumia maelfu ya dola kufanyia anasa za manunuzi ya vitu kwa kutumia fedha alizopewa na Agliotti.

Mawakili wa Selebi, washirika wa karibu wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, walisema kuwa alikuwa ni kafara wa mchezo wa kisiasa wa kumtafuta mchawi baada ya hasimu mkubwa wa Bw Mbeki, Jacob Zuma kuwa Rais mwaka 2009.

Lakini Jaji Joffe Meyer alitupilia mbali hoja hiyo na kumwelezea Selebi kama "mtu wa kudhalilisha" na "mgeni wa kusema ukweli" katika eneo la kutolea ushahidi.