Kesi ya Habre itaanza karibuni Senegal

Senegal inasema kuwa imejitolea kumfikisha mahakamani kiongozi wa zamani wa Chad, Hissene Habre, baada ya uamuzi uliotolewa Ijumaa na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC, mjini Hague.

Haki miliki ya picha Reuters

Serikali ya Senegal imekariri azma yake ya kufungua mashtaka kabla ya mwisho wa mwaka.

Bwana Habre ameishi nchini Senegal tangu alipopinduliwa mwaka wa 1990, lakini hadi sasa Senegal imeshindwa kumfikisha mahakamani.

Msemaji wa Wizara ya Sheria ya Senegal, Marcel Mendy, aliiambia BBC kwamba serikali inafanya kila iwezalo kuanzisha kesi ya kiongozi wa zamani wa Chad, ufikapo mwisho wa mwaka.

Msemaji huyo alieleza kuwa kamati ya utendaji ilianzishwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Kamati hiyo, pamoja na wataalamu wa sheria kutoka Umoja wa Afrika, watakutana katika siku chache zijazo kutengeneza mwongozo wa kufuatwa hadi kufikia kesi.

Chad, pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani, zimeahidi kusaidia kifedha kwenye gharama za kile Bwana Mendy alisema, itakuwa kuanzisha mahakama maalumu.

Mahakimu watatoka Senegal na kwengineko.

Alipochaguliwa awali mwaka huu, Macky Sall wa Senegal, alisisitiza kuwa Hissene Habre, anayetuhumiwa kubeba dhamana ya mauaji ya maelfu ya watu kwa sababu za kisiasa, na kuwaadhibu watu nchini Chad, anafaa kupelekwa mbele ya mahakama ya Afrika, siyo kupelekwa Ulaya.