Waasi wa M23 washambuliwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jean Marie Runiga kiongozi wa kisiasa wa chama cha M23

Vikosi vya majeshi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, vikisaidiwa na vikosi vya Umoja wa mataifa, wamewashambulia waasi na kuwafurusha kutoka mji muhimu wa Mashariki mwa nchi hio wa Goma.

Waasi wa vuguvugu la M23, ambao Umoja wa mataifa unasema wanafadhiliwa na Rwanda, walitisha wiki iliyopita kuuteka mjini wa Goma, ambao ni kituo muhimu cha jeshi la kitaifa.

Mapigano bado yanaendelea umbali wa kilomita hamsini kaskazini mwa Goma katika eneo la Rutshuru.

Mwandishi wa BBC katika eneo hilo anasema raia wengi wamehama makwao na kukimbilia mjini Goma na kutafuta afueni katika kambi za Umoja wa mataifa katika eneo hilo.

Mapigano haya mapya yalianza mwezi Aprili, huku serikali ya DRC ikituhumu jirani wake Rwanda kwa kuunga waasi mkono ingawa Rwanda imekanusha madai hayo.

Zaidi ya watu 200,000 wamepotza makao yao kufuatia vita hivyo.

Mwandishi wa BBC mjini Goma anasema kuwa mapigano sasa yako katika maeneo yanayozingira mji wa Rutshuru umbali wa kilomita 50 kaskazini mwa Goma.

Wananchi watoroka.

Hii ina maana kuwa majeshi ya serikali yakiungwa mkono na wanajeshi wa umoja wa mataifa, wameweza kuwafukuza waasi wa M23

Lakini huu ni mgogoro ambao hauna maeneo maalum ambako mashambulizi yanafanyika, inaarifiwa mashambulizi yanatoka pande zote.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wananchi watoroka vita mashariki mwa Congo

Raia wamekuwa wakikimbilia usalama wao na kutafuta hifadhi mjini Goma au katika sehemu zinzozingira kambi za vikosi vya amani vya umoja wa mataifa.

Uasi huu unaongozwa na mwanajeshi muasi Bosco Ntaganda, anayetuhumiwa na umoja wa mataifa kupokea usaidizi wa serikali ya Rwanda.

Ntaganda ni wa kabila la Tutsi sawa na ilivyo kwa viongozi wa Rwanda ambao wanahofia mashambulizi kutoka kwa kabila hasimu la wa Hutu wanaoishi mashariki mwa DR Congo.

Eneo la Mashariki mwa DR Congo limekumbwa na mapigano makali tangu mwaka 1994,wakati zaidi ya wa Hutu milioni moja walivuka mpaka na kuingia DR Congo baada ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.

Rwanda imeweza kushambulia DRC mara mbili ikisema kuwa ilikuwa inavamia waasi wa ki Hutu walio nchini humo.