Je kutakuwa na mauji ya halaiki Aleppo?

Marekani imeelezea kuwa ina hofu kwamba Syria inajiandaa kutekeleza mauaji ya halaiki katika mji wa Aleppo.

Wizara ya mambo ya ndani ya Marekani imesema kuwa ripoti zakuaminika zinaashiria kuweko kwa msururu wa vifaru vya kijeshi vinavyoelekea katika mji huo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mapigano katika mji wa Aleppo, Syria

Waasi nchini Syria wanasema kwa sasa wanathibiti zaidi ya nusu ya sehemu ya mji wa Aleppo, lakini dalili zote viungani mwa mji huo zinaashiria kutokea kwa mapambano makubwa zaidi ambayo haijabainika mshindi atakuwa nani.

Raia wengi wanatarajiwa kujikuta katikati ya vita hivyo na chakula, maji, dawa na umeme vimekuwa haba. Vikosi vya serikali vimekuwa vikielekea katika mji huo na wanaharakati wanasema wanajeshi zaidi wako njiani.

Pande zote mbili zimeripoti kutokea mapigano lakini bado hapajatokea shambulio kubwa.

Wanaharakati wametuma picha za video kwenye mtandao wa internet zikionyesha basi lililoteketezwa na miili ya watu iliyotekeketea baada ya kushambuliwa kwa risasi.

Wanaharakati hao wamesema miili hiyo ni ya watu waliouwawa kinyama na jeshi la wanahewa baada ya kuzuiliwa.

Katika mji wa Damascus, milipuko mikubwa imesikika huku mapigano yakiripotiwa wakati wanajeshi wakijaribu kuwatimua wapiganaji wa upinzani katika maeneo ya kusini mwa mji huo na karibu na kambi mbili za wakimbizi wa kipalestina.

Wakati hayo yakiarifiwa wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Syria imethibitisha, lakini ikapuuzilia mbali kujiuzulu kwa wanadiplomasia watatu zaidi.

Wanadiplomasia hao ni kaimu mkuu wa ujumbe wa Syria nchini Cyprus, mme wake ambaye alikuwa balozi wa Syria katika milki za kiarabu na afisa mmoja katika ubalozi wa Syria nchini Oman.

Wizara hiyo imeilaumu Qatar kwa kufadhili na kuwahimiza maafisa wa serikali kujiuzulu.