Maelfu ya Waethiopia wakimbilia Kenya

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, linasema kuwa watu zaidi ya 20,000 wamekimbilia Kenya, baada ya mapambano katika mji ulioko kwenye mpaka wa Ethiopia na Kenya.

Haki miliki ya picha s

Mapigano yalianza Jumatano, baina ya makabila mawili, karibu na mji wa Moyale.

Inafikiriwa kuwa watu kama 18 wameuwawa.

Taarifa kutoka eneo hilo zinasema hali sasa imedhibitiwa.

Mapigano yalianza kati ya juma, na chanzo kilikuwa mzozo wa muda mrefu kuhusu ardhi baina ya makabila mawili.

Taarifa kutoka huko zinaeleza kuwa wanamgambo waliokuwa na silaha walijizatiti Jumatano, na mapigano yakatapakaa haraka hadi mji wa mpakani, Moyale.

Aliyeshuhudia tukio hilo aliiambia BBC kwamba wanajeshi wa serikali ya Ethiopia waliingilia kati kuzima fujo siku ya Ijumaa.

Lakini ingawa viongozi wa eneo hilo wamewaomba watu warudi makwao, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya linasema watu wengi bado wanavuka mpaka na kuingia Kenya.