Ebola Uganda ilianza kwa mja mzito

Wizara ya Afya ya Uganda imetangaza kuwa ugonjwa wa Ebola umeibuka tena, na wakuu wa afya wanasema hadi sasa umeuwa watu 13, na watu 7 wengine wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo.

Haki miliki ya picha online

Maafisa wanasema ugonjwa huo ulijitokeza mwezi wa Juni, na wanajitahidi kuudhibiti usitapakae.

Wakuu wanasema mtu wa kwanza kufa kwa ugonjwa huo ni mwanamke mja mzito, ambaye alitanguliwa na mtoto wake mchanga, na yeye mwenyewe punde akamfuata.

Wanasema watu wengi waliokufa walikuwa jamaa wa karibu, ambao waliambukizwa mazikoni au wakati wanawauguza wagonjwa.

Wagonjwa wengi ni kutoka wilaya ya Kibaale, jimbo la magharibi mwa Uganda.

Wizara ya Afya inasema imechukua hatua za dharura katika eneo hilo, na imewasihi wenyeji wa huko waepuke mikusanyiko mikubwa ya watu, hasa mazishi.

Tangu mwaka 2,000 ugonjwa wa Ebola umeshajitokeza mara tatu nchini Uganda.

Na wizara ya Afya inamchunguza mgonjwa mmoja ambaye wanafikiri anauguwa Ebola, katika hospitali ya rufaa ya Mulago, mjini Kampala.

Dr Anthony Mbonye, mkuu wa idara ya afya ya jamii, anasema wakuu wanajitahidi kuhakikisha kuwa ugonjwa hautatapakaa katika hospitali hiyo.