Saif Islam: 'kesi isikilizwe Hague'

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Saif Islam ataka kesi yake kusikilizwa The Hague

Mtoto wa Kanali Gaddafi amesema anataka kesi yake iendeshwe The Hague, badala ya kuendeshwa nchini Libya, mawakili wake wamesema.

Saif al-Islam alisema iwapo kesi yake itaendeshwa Libya basi inakuwa sawa na kuuawa, kwa mujibu wa nyaraka zilizowasilishwa mahakama ya ICC.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 40 anashikiliwa na wapiganaji mjini Zintan. Amekuwa akishikiliwa Libya tangu Novemba 2011

Alishtakiwa na ICC kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Serikali ya mpito ya Libya mpaka sasa imekataa kumkabidhi Saif Uholanzi ambako mahakama ya ICC iko ikisema kuwa hana budi kukabiliana na mashataka yake nchini Libya.

Kanali Gaddafi, ambaye utawala wake wa kidikteta ulidumu kwa miaka 42 aliuawa katika mazingira ya kutatanisha baada ya kukamatwa na waasi mwezi Octoba, katika kitendo ambacho kilishutumiwa vikali na makundi ya haki za binadamu.

'Ulinzi wa bandia'

"Siogopi kufa lakini ikiwa itaendeshwa hapa hiyo muuite tu kuwa ni uuaji na mmalizane," Saif al-Islam alinukuliwa na mawakili akisema.

Mwezi Juni, wafanyakazi waliotumwa na ICC walikamatwa baada ya kukutana na Saif al-Islam, na kushikiliwa kwa zaidi ya wiki tatu.

Nyaraka zilizowasilishwa mahakamani zinasema wakati wa mkutano huo afisa aliyejifanya mlinzi alimzuia mwanasheria wa ICC kuchukua kiapo kutoka kwa Saif al-Islam.

"Mlinzi huyo ambaye kimsingi ni Bw Ahmed Amer – mwanasheria anayezungumza lugha kadhaa alijumuishwa kwenye timu hiyo makusudi kuwalaghai " nyaraka ziliandika, kwa mujibu wa Reuters.

"Alirejea chumbani na (mkalimani wa ICC akiwepo) alianza kupiga kelele kuwa maelezo hayo yalikuwa hatari sana, yamekiuka usalama wa Libya na kwa Ulinzi wasingeyarudisha"

Mkutano ulistishwa baada ya dakika 45 na nyaraka zao kuharibiwa, wakili alisema. Baadaye walikamatwa.

Hatua hiyo ilionekana kuwa "kimyume cha sharia, uhaini na ukiukwaji wa taratibu za usalama wa Taifa kwa ama Bw Gaddafi au washauri wake na kuonyesha kuwa Gaddafi hataki kesi yake iendeshwe na mahakama za Libya." Walisema mawakili kwenye nyaraka.

Maafisa wa Libya walimshutumu wakili Melinda Taylor, aliyekuwa akiongoza ujumbe wa ICC, kwa kuwa na vifaa vya upelelezi vikiwa vimeshikizwa kwenye barua ya Saif al-Islam wakati wa mkutano.