Ezekiel Kemboi kidedea!

Bingwa wa dunia katika mashindano ya mbio za mita 3000 kuruka viunzi na kidimbwi cha maji Ezekiel Kemboi aliinyakulia Kenya medali ya Kwanza ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki mjini London Uingereza.

Kemboi mwenye umri wa miaka 30, alikamilisha mbio hizo katika muda wa dakika 8 na mishale ya sekunde18.56, huku Mahiedine Mekhissi-Benabbad wa Ufaransa akiridhika na nishani ya fedha.

Image caption Mkenya Ezekiel Kemboi

Na kama ilivyo dasturi, Ezekiel Kemboi alisakata rumba mbele ya kadamnasi ya watu kusherehekea ushindi wake.

Mkenya Abel alinyakuwa nishani ya shaba lakini palikuwa na vurumai baadaye ya mkenya mwenzake Brimin Kipruto kutegwa ikiwa imesalia mita 700 mbio hizo kukamilika.

Kipruto alifanikiwa kunyanyuka mara moja lakini akaambulia katika nafasi ya tano.

Kenya imekuwa ikitawala mbio hizi katika mashindano ya Olimpiki, na mara hii mambo yalikuwa ni hayo hayo.

Bwana ya kuanza mbio hizo kwa mwendo wa aste aste Kemboi, ambaye pia alinyakuwa ubingwa Olimpiki mwaka 2004, alichukuwa usukani katika mzunguko wa mwisho.

Kisha akatimuka katika hatua za mwisho na kuwaacha wanariadha wenzake hatua kadhaa nyuma. Ikawa kazi mboga kwake kuugusa utepe.

Mwanariadha huyo machachari akapamba ushindi wake kwa kulisakata rumba uwanjani mbele ya mashabiki alfu 80,000 katika uwanja wa Olimpiki mjini London.