Mashambulizi makali yatokea Ivory Coast

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wa Ivory Coast waliouawa

Majambazi waliokuwa wamejihami wameshambulia kambi ya kijeshi mjini Abidjan, mji mkuu wa Ivory Coast na kuwaua takriban wanajeshi sita.

Wenyeji walielezea kusikia milio ya risasi usiku kucha katika mtaa wa Riviera. Idadi kubwa ya wanajeshi wakiwemo walinzi wa amani wa umoja wamataifa, wamepelekwa katika eneo hilo ingawa sasa maafisa wakuu wanasema kuwa hali imeweza kudhibitiwa.

Mji huo ulishuhudia mapambano makali, mwaka jana wakati wa mvutano wa kisiasa ambao ulitokea baada ya matokeo ya uchaguzi ambayo yalizua utata mkubwa.

Mnamo siku ya Jumapili, wapiganaji waliokuwa wamejihami walishambulia kizuizi cha jeshi barabarani katika eneo la Yopougon mashariki mwa Ivory Coast pamoja na kituo cha polisi na kuwaua wanajeshi watano katika kambi ndogo ya kijeshi mjini Abidjan.

Wapiganaji hao walivalia sare za kijeshi na kutumia silaha nzito nzito japo hawakuweza kutambuliwa.

Milio ya risasi pia ilisikika mwishoni mwa wiki katika eneo la Abengourou mashariki mwa nchi na sababu ya shambulio aijajulikana.

Shambulio hilo lilitokea katika wilaya ya Yopougon ambayo inaaminiwa kuwa mojawapo ya wilaya zilizoshambuliwa zaidi na waasi wakati wa machafuko na hatimaye ushindani wa uongozi wa Abidjan kufuatia matokeo yaliyozua utata wa uchaguzi wa urais mwaka jana.

Maiti wanne walionekana katika mlango wa jengo moja katika kambi ya jeshi ya Akouedo huku damu ikionekana imetapakaa kwenye sakafu na hata kwenye ukuta. Mlango huo ulikuwa umevunjwa. Miili mingine miwili ilipatikana katika lango lengine kubwa.