Kikosi cha pamoja kutumwa DRC

Viongozi wa mataifa ya eneo la maziwa makuu walioko mjini Kampala kwa kikao cha kutafuta suluhisho la mzozo wa kivita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, wamekubaliana kuunda jeshi la pamoja kulinda usalama katika eneo la mashariki mwa DRC.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mapigano Mashariki mwa DRC yamesababisha wengi kutoroka makwao.

Baada ya kikao kilicho kufunguliwa jana na rais Yoweri Museveni wa Uganda na kuhudhuriwa na marais watano kutoka mataifa ya eneo la maziwa makuu ni moja ya mikakati ya kumaliza mzozo wa mashariki mwa Kongo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kampala, waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uganda Oriem Okelo, amesema mataifa wanachama yamekubaliana kubuni jeshi la pamoja kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Lakini amesema mawaziri wa ulinzi kutoka mataifa hayo watakutana kuchukuwa uamuzi wa mwisho kuhusu kubuniwa kwa jeshi hilo.

''kikosi kitakachobuniwa kitakuwa kama kile cha Umoja wa Mataifa au Umoja wa Afrika na ni sharti Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zikubaliane,'' amesema Bw. Okelo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jean Marie Runiga, kiongozi wa mrengo wa kisiasa wa kundi la waasi wa M23

Mkutano huo wa mawaziri wa ulinzi utafanyika tarehe 15, mwezi huu wa Agosti.

Bwana Okelo amesema marais wa Rwanda Paul Kagame na Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameafikia makubaliano na sasa ''wanazungumza kwa simu na hawana matata.''

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Rais Paul Kagame anashutumiwa kuunga mkono kundi la M23

Mwenyekiti wa kikao hicho cha viongozi wa eneo la maziwa makuu rais wa Uganda Yoweri Museveni alifanya kikao cha faragha na Bw. Kagame anayeshutumiwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa kutoa msaada kwa waasi wa M23 katika eneo la mashariki mwa DRC.

Kadhalika alifanya mashauri na Bw. Kabila.

Kabla ya kikao hicho kinachokamilika leo hii kuanza, Bw. Museveni, baada ya ufunguzi rasmi aliwaagiza waandishi wa habari kuondoka mara moja na pia kuliagiza shirika la utangazaji nchini Uganda UBC kutopeperusha yale yaliyokuwa yakijadiliwa katika mkutano huo moja kwa moja.

Mwandishi wa BBC mjini Kampala anasema hiyo ni dalili kuwa huenda kulikuwa na ubishi mkali katika mkutano huo.