Obama aomboleza kifo cha Armstrong

Imebadilishwa: 26 Agosti, 2012 - Saa 10:33 GMT
Neil Armstrong

Neil Armstron alikuwa mtu wa kwanza kukanyaga mwezini mwaka 1969

Rais wa Marekani, Barack Obama, ameiongoza nchi hiyo katika kuomboleza kifo cha mtaalamu wa anga za juu, Neil Armstrong, na aliyekuwa mtu wa kwanza kukanyaga mwezini, ambaye alifariki Jumamosi akiwa na umri wa miaka 82.

Kupitia mtandao wa jamii wa Twitter, Obama aliandika: "Neil Armstrong sio tu alikuwa shujaa katika enzi yake, bali alikuwa shujaa wa enzi zote".

Mamilioni ya watu kote duniani walimtizama Armstrong alipotua mwezini tarehe 20 Julai, mwaka 1969, na wengi wanayakumbuka matamshi yake alipoelezea kwamba hiyo ilikuwa ni "hatua moja kwa binadamu, lakini hatua nyingi mno kwa maendeleo ya binadamu", akimaanisha ufanisi mkubwa uliopatikana kisayansi.

Matamshi hayo yakawa ni kati ya maneno muhimu sana yaliyonakiliwa na wengi mara kwa mara katika karne ya 20.

Familia ya Armstrong ilithibitisha kifo chake kupitia taarifa siku ya Jumamosi, ikielezea kwamba alifariki baada ya matatizo yaliyojitokeza kufuatia upasuaji wa mishipa minne ya damu.

Taarifa hiyo ilimsifu kama Mmarekani shujaa, lakini mtu ambaye hakutaka kujigamba, na wakitaka waliomsifu kuiga mfano wake, kwa kutoa huduma na kupata ufanisi, huku wakiwa wanyenyekevu.

"Wakati unapokuwa ukitembea usiku, na hali ya anga ikiwa nzuri, basi unapoutizama mwezi ambao unatabasambu, ukonyezee jicho, na umkumbuke Neil Armstrong," familia yake ilielezea kupitia taarifa.

Bw Obama alimshukuru Armstron kwa kuwawezesha binadamu ufanisi mkubwa wa "hatua hiyo moja".

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.