Hofu yaendelea mgodini Afrika Kusini

Imebadilishwa: 27 Agosti, 2012 - Saa 12:55 GMT

Polisi walipokuwa wakiwakabili wachimba madini wakati wakiandamana mgodini Marikana

Wachimba madini wanaofanya kazi katika mgodi wa Marikana Afrika Kusini walipouawa wengine 34 kwa kupigwa risasi na polisi, wamekuwa wakipewa vitisho kuwazuia kurejea kazini.

Kampuni ya mgodi huo ya Lonmin inasema ni asilimia 13 tu ya wafanyakazi walioripoti kazini siku ya Jumatatu kutokana na wengi kutishiwa.

Mamia ya wachimba madini wanaripotiwa kukusanyika nje ya mgodi huo, huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi.

Viongozi wa chama tawala cha ANC wanatarajiwa kufanya mazungumzo kujadili mauaji hayo.

ANC imekuwa ikishutumiwa kwa kushindwa kushughulikia mgogoro huo ipasavyo, na rais Jacob Zuma anatarajiwa kuulizwa maswali mazito katika mkutano huo ambao vyombo vya habari havijakaribishwa rasmi.

Lonmin ambayo ni ya tatu kwa ukubwa ulimwenguni kwa uzalishaji wa madini ya dhahabu nyeupe, ilitarajia mgomo katika mgodi huo ungemalizika na uzalishaji kurejea kama kawaida.

''Wafanyakazi wanasubiri mazingira yawe salama. Makundi ya watu yamekuwa yakipita kutishia watu wanaokuja kazini,'' msemaji wa Lonmin Sue Vey ameiambia BBC.

Mauaji hayo yameitikisa nchi hiyo, Alfonso Mofokeng mchimba madini kutoka Lesotho aliliambia shirika la habari la AFP:

Rais Jacob Zuma alipokuwa akizungumza na wachimba madini waliogoma tarehe 22 Agosti

''Tunajua kwamba kuna baadhi ya watu wamerejea kazini, tunahitaji kuja na njia ya kuwashughulikia.''

Asilimia 13 ya waliohudhuria kazini ni pungufu sana ya ile asilima 30 ya waliohudhuria wiki iliyopita na pia asilimia 57 mwishoni mwa wiki.

Shughuli katika migodi ya Lonmin zimesimama maeneo mbalimbali tangu mgomo wa kudai malipo zaidi na mazingira bora zaidi ya kazi kuanza mapema mwezi huu, na hivyo kusababisha bei ya madini hayo kupanda.

Wakati huohuo uchunguzi umeanza kuhusu shutuma za baadhi ya wachimba madini kudhalilishwa walipokuwa katika kizuizi cha polisi, msemaji wa Kitengo huru cha uchunguzi wa polisi (Independent Police Investigative Directorate-IPID) ameithibitishia BBC.

Moses Dlamini amesema baadhi ya watu wamesema walipigwa ili kuwalazimisha kuwahusisha wenzao na vifo vya polisi wawili vilivyotokea kabla ya mauaji ya wachimba madini.

Amesema wengine wanasemekana kudhalilishwa kwasababu walitoa maelezo kwa waliokuwa wakifanyia uchunguzi mauaji hayo.

Ameongeza kuwa IPID inachukuliwa vifo vya wachimba madini 34 kama kosa la mauaji.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.