Romney mgombea wa urais chama cha Republican

Imebadilishwa: 29 Agosti, 2012 - Saa 07:04 GMT

Mitt Romney na mkewe Ann

Mitt Romney ameteuliwa rasmi kama mgombea urais wa chama cha Republican katika kongamano la chama hicho huko Tampa, Florida.

Wajumbe kutoka majimbo yote ya Marekani walikusanyika kuthibitisha kumuunga mkono gavana huyo wa zamani wa jimbo la Massachusetts.

Atakabiliana na Barack Obama katika uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba.

Kura ya maoni ya hivi karibuni inaonyesha wagombea hao wawili Bwana Romney na rais Obama wakipimana nguvu kwa karibu.

Bwana Romney, 65, alihitaji kupata japo kura za wajumbe 1,144 ili aweze kuteuliwa kama mgombea wa chama chake, na kura za kutoka jimbo la New Jersey zilimuweka "katika nafasi nzuri".

Dakika chache baadaye, mjumbe wa bunge la congress wa Wisconsin Paul Ryan akateuliwa rasmi kuwa mgombea wa kiti cha makamu wa rais wa chama cha Republican.

Fursa ya Ann Romney

Bwana Romney aliteuliwa na wajumbe ambao walikuwa wakitangaza kura za majimbo yao kwa sauti hadharani.

Kwa ujumla, Bwana Romney alipata kura 2,061, Spika wa bunge la waakilishi John Boehner alitangaza katika kongamano hilo.

Bwana Romney hakuwepo kwenye kongamano hilo, lakini alifuatilia kuhesabiwa kwa kura akiwa katika hoteli ya karibu yeye na mkewe.

Uteuzi wake huko Tampa unathibitisha rasmi kuidhinishwa na chama chake kufanya kampeni.

Waliozungumza kwenye kongamano hilo walimshambulia rais Obama.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya chama cha Republican Reince Priebus alisema rais hajawahi "kusimamia kampuni. Hajawahi hata kusimamia karakana."

Wakati huo huo, Bwana Boehner amesema: "utendaji kazi wa rais Obama si wa kiwango cha kusifiwa."

Siku ya Jumanne jioni, Ann Romney pia pamoja na Gavana wa jimbo la Carolina Kusini Nikki Haley na Gavana wa jimbo la New Jersey Chris Christie walizungumza.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.