Hukumu ya haki kwa Abdullah Senussi

Imebadilishwa: 6 Septemba, 2012 - Saa 14:20 GMT

Abdallah al-Senussi

Marekani pamoja na mashirika mbali mbali ya kutetea haki za binadamu, imeitaka serikali ya Libya kumfanyia hukumu ya haki mkuu wa zamani wa ujasusi nchini Libya Abdullah al-Senussi.

Serikali ya Mauritania ilimkabidhi Senussi kwa maafisa wa utawala wa Libya siku ya Jumatano.

Marekani imesisitiza kuwa lazima kesi ya Abdullah al-Senussi ifanywe kuambatana na sheria za kimataifa.

Waziri mkuu wa Libya, naye alisema kuwa bwana Senussi atafunguliwa mashtaka na kesi yake kuendeshwa kulingana na sheria za kimataifa bila kukiuka haki za binadamu.

Libya inataka kumfungulia mashtaka bwana Senussi kwa makosa aliyoyafanya chini ya utawala wa hayati Muamar Gaddafi.

Mapema mwezi huu Rais wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz alisema kuwa bwana Senussi aliyekuwa amekimbilia nchini humo, sharti kwanza akabiliwe na sheria kwa makosa ya kuingia Mauritania kinyume na sheria.

Senussi alitoroka Libya baada ya mapinduzi ya mwaka jana ambayo yalimng'oa mamlakani hayati Gaddafi.

Pia anatakiwa na Ufaransa pamoja na mahakama ya kimataifa ICC kwa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ripoti za kukabidhiwa kwake kwa watawala wa Libya, zilitolewa na televisheni ya taifa pamoja na shirika rasmi la habari la Mauritania.

Kulingana na ripoti, bwana Senussi alikabidhiwa kwa wajumbe wa Libya walioongozwa na waziri wa sheria na haki wa nchi hiyo. Lakini hadi sasa bwana Senussi hajulikani aliko.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.