Malema awashauri wanajeshi kudai haki zao

Imebadilishwa: 12 Septemba, 2012 - Saa 14:32 GMT

Mwanaharakati wa kisiasa nchini Afrika Kusini Julius Malema, amewashauri wanajeshi wenye manung'uniko kujipanga vyema na kupigania kazi zao.

Malema aliyatoa matamshi hayo kwa wanajeshi wanaokabiliwa na makosa ya kinidhamu yaliyotokana na maandamano waliyoyafanya mwaka 2009 wakidai mishahara mizuri na mazingira bora ya kazi.

Kambi za jeshi leo ziliwekwa katika hali ya tahadhari kabla ya hotuba yake kwa wanajeshi hao, ikiwa ndio mara ya kwanza hatua kama hii kuchukuliwa tangu kumalizika kwa enzi ya ubaguzi wa rangi.

Bwana Malema ni mwanasiasa anayeibua mgawanyiko hapa. Hivi maajuzi alifukuzwa kutoka chama cha ANC na kwa sasa anafanyiwa uchunguzi kuhusiana na kashfa ya ufisadi.

Lakini hajaondoka ANC kimya kimya. Badala yake ametumia mauaji ya hivi maajuzi katika mgodi wa Marikana kuanzisha kampeni kali dhidi ya mabepari nchini Afrika Kusini na kutaka yafanyike mapinduzi ya kiuchumi.

Wengi wanamshutumu kwa kuhusika na ubinafsi mbaya wa kisiasa, lakini malema anapokea uungwaji mkubwa kutoka kwa jamii za watu maskini na kimya cha serikali ni ishara tosha kuwa imeshindwa kukabiliana naye.

Manung'uniko ya wanajeshi ni fursa nyingine kwa Malema kuonyesha ubabe wake na hali ni tete nchini Afrika Kusini.

Hofu iliyopo ni kwamba migomo huenda ikaenea zaidi na kwamba serikali kwa sasa inazingirwa na migogoro ya ndani huku baadhi ya mirengo serikalini ikipanga njama ya kumtimua madarakani rais Jacob Zuma.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.